Maswali

1. Je tatizo hili litatokea tena?

Mara likiisha kutokea, uwezekano wa kutokea tena huongezeka kwa asilimia 10. Kwa ujumla, jamii nzima iko katika hatari ya kati ya asilimia 1 na 2. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa uwezekano wa kupata mimba kwa kawaida baada ya tatizo hili si mbaya kwani upo kati ya asilimia 50 na 80.

2. Je uwezekano wangu wa kupata mimba kwa njia ya kawaida ukoje?

Kwa ujumla uwezekano huu hubakia kuwa kati ya asilimia 50 na 80. Kama nilivyoeleza hapo juu hatari ya kujirudia kwa tatizo katika jamii huwa ni kati ya asilimia 1 na 2. Endapo mimba yako ilikuwa ni ya kupandikizwa, uwezekano wa mimba ya kawaida hupungua kwani hatari ya mimba nje ya mirija ya uzazi na mimba kutoka katika kundi hili la wagonjwa ni mkubwa. Hatari ya mimba nje ya mirija ya uzazi baada ya kupandikiza mimba kwa wastani huongezeka mara 4. Ukiweza kupaata mimba ikashika sawasawa katika jaribio la kwanza, basi unaweza kukuza mimba yako kikawaida kama mtu yeyote yule. Hatari ya mimba nje ya mirija ya uzazi haitasababisha mimba, uchungu au kujifungua kuwa na matatizo ya ziada. Hakuna sababu ya kumwona mkunga mara kwa mara eti tu kwa sababu uliwahi kupata mimba nje ya mirija ya uzazi.

3. Je ni lini nitaacha kwenda mwezini/kivuja?

Swala la uvujaji au kwenda mwezini baada ya mimba nje ya mirija ya uzazi huwa wa kawaida tu. Hii inatokana na kuchunika kwa ngozi kwenye nyumba ya uzazi.. Haitegemewi kuchukua muda mrefu zaidi. Hata hivyo upo uwezekano wa kupata kipindi kirefu zaidi. Kama una wasiwasi zaidi onana na daktari.

4. Je ni lini yanipasa kujaribu tena kupata mimba?

Hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ukijaribu kupata mimba mapema baada ya mimba nje ya mirija ya uzazi kuna hatari ya kupata tatizo hilo tena. Kama ulitibiwa kwa dawa iitwayo “methotrexate”, unashauriwa kusubiri kwa miezi mitatu kwa sababu tiba hiyo ina vijimelea vinavyosababisha kuchelewa kwa ukuaji wa mtoto hasa kwenye siku za mwanzo. Tumia salama za kutosha wakati ukisubiri.

5. Niliambiwa na daktari kuwa nina ‘Salpingostomy’, je ni nini hii?

Salpingotomy ni pale mkato mdogo hufanywa kwenye mrija wa ‘fallopian’ ili kuondoa mimba nje ya mirija ya uzazi. Mrija hauondolewi ila ule mkato mdogo hubaki ukiunganika na kupona. Njia hii hushauriwa endapo mrija mwingine una matatizo.

6. Nilipofanyiwa upasuaji, mrija wote wa kushoto uliondolewa. Je kama kipande tu cha mrija kingeondolewa uwezekano wa kutunga mimba nyingine ungeongezeka?

Ushahidi unaonyesha kuwa uwezekano wa mimba unabakia palepale. Hakuna tofauti kati ya mtu aliyetolewa kipande chote na yule aliyetolewa sehemu ndogo tu.

7. Kwa vile mimba yangu nje ya mirija ya uzazi ilipasuka nilipofanyiwa upasuaji usio wa kawaida badala ya ‘key hole’. Je, hii itanipunguzia uwezekano wa mimba nyingine?

Upasuaji wa ‘laporascopic key hole’ una manufaa ya kufungua sehemu ndogo tu ya utumbo na hivyo kupona haraka. Hakuna ushahidi kuonyesha kuwa njia moja au nyingine ya upasuaji inaingiliana na upataji au uzuiaji wa mimba zaidi.

8. Je kipindi changu cha mwezi kitarudi lini?

Kama ulikuwa na vipindi vya kawaida kabla ya mimba, basi tegemea kuanza tena kati ya wiki 4 hadi 6. Hii inaweza kuwa tofauti kulingana na ratiba yako ya awali. Endapo muda huu utapita bila chochote na unakuwa na wasiwasi, basi mwone daktari.

9. Je itakuwaje kama ‘rhesus’ yangu ni hasi?

Iwapo hii ni mimba ya kwanza, itabidi upewe ‘Anti-D’ ndani ya kipindi cha siku 3 za matibabu kwa kudungwa sindano. Kama hujui kundi la damu yako mwuulize daktari anayekutibu kwani damu yako huangaliwa mara kwa mara unapokuwa na mimba nje ya mirija ya uzazi.

10. Je waweza kufanya lolote ili kuzuia mimba nyingine nje ya mirija ya uzazi?

Jibu ni hakuna. Mpaka sasa hakuna dawa iliyopatikana na wala kuondoa mirija hakuasaidii. Njia bora ni kutumia njia madhubuti za kuzuia mimba. Kama unadhani una maambukizi yoyote yale, mwone daktari. Kama utapata mimba ni muhimu kukumbuka kuwa uko katika hatari zaidi ya kuwa nje ya mirija ya uzazi. Utambuaji wa mapema ni muhimu ili kupata matibabu.

11. Je naweza kupata IUCD? (Intrauterine Contraceptive Device).

Ni salama kutumia IUCD kama uliwahi kupata mimba nje ya mirija ya uzazi. ‘Coil’ ya shaba pamoja na ‘mirena’ vyote vinafaa na salama. Hata hivyo endapo vifaa hivyo vitapata mushkeri, basi hatari ya mimba nyingine nje ya mirija ya uzazi huongezeka.

12. Je naweza naweza kutumia ‘Mini – Pill’?

Jibu lake ni sawa na jibu la swali la 11 hapo juu.

13. Je mtoto wangu anayefuata hatakuwa wa kawaida?

Kupata mimba nje ya mirija ya uzazi si lazima kusababishe wewe kuwa na matatizo ya mimba baadaye. Kama umetibiwa kwa dawa ya ‘Methotrexate’ yafaa usubiri miezi 3 kabla ya kujaribu kupata mimba nyingine na kama ukipata mimba ndani ya miezi mitatu basi umwone daktari wako ambaye atakupeleka kwa wataalam zaidi kwa uchunguzi. Jadiliana kwa kirefu na mtaalam.

14. Je ni fanyeje kipimo cha mimba kikiwa chanya?

Ni muhimu sana kumwona daktari kwa ushauri kwenye wiki ya 5 hivi. Daktari anaweza kukupeleka kwenye hospitali ya jirani kwa ajili ya ‘ultra sound’ ya mapema. Itakuwa ni vema endapo utafanyiwa uchunguzi wa ndani ya kizazi. Hii hutoa uhakika zaidi. Kama haifahamiki vizuri mimba ilipokaa, basi ufuatiliaji wa karibu utahitajika.

15. Je nitajifungua kwa kupasuliwa?

Hakuna ushahidi kuonyesha kuwa utalazimika kuendelea kuzaa kwa kupasuliwa wakati wote eti kwa sababu uliwahi kupata mimba nje ya mirija ya uzazi. Kama utachagua mwenyewe kuzaa kwa kupasuliwa, hatari ya kupata mimba nje ya mirija hongezeka kiasi. Hii ni kwa sababu uwezekano wa maambukizi ya vijidudu huwa ni mkubwa kuliko kuzaa kwa kawaida.

Translated by: Mary Mclachlan, SHO O & G, WGH
Mary- Stella Kivali, Staff Nurse, WGH